Thursday, October 23, 2008

HUU UCHAFU BONGO

Licha ya msongamano wa watu na foleni za magari bado ipo sifa moja kubwa ya uchafu katika jiji la Dar es salaam. Ni sifa ambayo wengi wetu huisahau katika wasifu wa jiji hili la Dar es salaam, lakini pindi unaposhuka ubungo kutoka mikoa mingine au nchi jirani ni lazima uso wako utakutana na uchafu mwingi unaotabasamu huku ukikukaribisha kwa mbwembwe ukisema “karibu mgeni”.

Ingawa kwa kiwango fulani serikali inajitahidi kuliweka jiji katika hali ya usafi ikiwa ni pamoja na kuweka mabango sehemu mbalimbali za jiji yakiwa na ujumbe wa “weka jiji safi” na kuweka ndoo maalum kwa ajili ya kuwekea uchafu sehemu mbalimbali za jiji ili kuimarisha usafi na hata baadhi ya daladala kuwa na ndoo hizo lakini bado haijafanikiwa kwa kiwango cha kuridhisha, kutokana na uchafu kuzidi kutapakaa kila kona ya jiji na mlipuko wa magonjwa yatokanayo na uchafu ukiwemo ugonjwa wa kipindupindu ambao hushambulia kwa kasi jiji hili kila mwaka kasi ambayo naweza sema kuwa ni kubwa ukilinganisha na mikoa mingine.

Harufu mbaya hutawala maeneo mengi ya jiji kutokana na uchafu, hususan kipindi cha mvua ambapo wakazi wengi wa jijini hufungulia maji machafu ya chooni ili kukwepa gharama za unyonyaji wa maji hayo, jambo ambalo huhatarisha afya na pia ni kero kwa wapita njia na wakazi jirani wa maeneo hayo.

Tatizo bado ni kubwa na mbaya zaidi uchafu huo huzagaa hadi maeneo ya posta ambapo ofisi kubwa za serikali zipo maeneo hayo zikiwemo wizara nyeti hapa nchini.

Imekuwa ni kitu cha kawaida kukutana na uchafu katika sehemu za soko na hata katika migahawa mbalimbali ya jijini ambapo mara nyingi mteja hukaribishwa kwa nderemo na vifijo vya wadudu inzi. Ni jambo la aibu sana kwa watanzania lakini limeshazoeleka na kuonekana kama ni sehemu muhimu ya maisha ya jijini.

Japokuwa watanzania hawana desturi ya usafi lakini umasikini nao unachangia kuongezeka kwa uchafu jijini. Kutokuwepo kwa vyoo vya umma vinavyotoa huduma bure kunasababisha ongezeko la uchafu.

Serikali inapiga kelele juu ya uchafu lakini inasahau kuwa si watanzania wote wenye uwezo wa kumudu gharama za choo. Kwa muuza maji, mpiga debe na watu wengi wasio na ajira kamwe hawataweza kulipia sh 100 kwa ajili ya kwenda msalani kujisaidia.

Ikiwa mtu anapata sh 500 kwa siku pesa ambayo haitoshi hata mlo wa siku moja ni wazi kuwa mtu huyo anapotaka kwenda msalani atapita uchochoroni na kufanya mambo yake. Ndiyo maana unapopita katikati ya jiji harufu ya mikojo na kinyesi ni jambo la kawaida kwa wakazi wa jijini. Kama serikali haitajenga vyoo vya umma sura mpya ya usafi katika jiji hili itakuwa ni ndoto.

Mamlaka ya maji safi na maji taka ina huduma ambazo zimelenga kwa watu wa hali ya juu, daima mwananchi wa kawaida hatoweza kunufaika na huduma hizi kutokana na gharama kubwa za utumiaji.

Harufu mbaya waipatayo wananchi hawa kutokana na kufungulia maji machafu ya chooni ili yasafirishwe na mvua, haiwafurahishi na kila mara serikali hukemea tatizo hili. Lakini ukemeaji wake hubaki kuwa wa mdomoni usiokuwa na utendaji.

Huduma nyingi za utoaji wa maji taka katika jiji la Dar es salaam hugharimu kati ya sh 25,000 hadi 70.000. ni watanzania wangapi wenye uwezo wa kumudu gharama hizo? Serikali au mamlaka husika imeweka mkakati gani ili kuwasaidia watu wa kipato cha chini ambao hupata chini ya dola moja kwa siku?

Kama huduma hii ingetolewa bure au kwa kiwango cha kumfanya kila mtanzania hasa yule anayeishi chini ya dola moja kwa siku aweze kumudu gharama hakuna mtu ambaye angefungulia maji hayo ili apate upepo wa kinyesi na kuhatarisha afya yake.

Kwa mamlaka ya maji safi na maji taka kuweka eneo la maji taka karibu na makazi ya watu maeneo ya buguruni kunamaanisha kuwa hata wahusika wa usimamizi wa mradi huu hawana uelewa juu ya usafi wa mazingira. Japokuwa walidai kuwa eneo hilo liliwekwa kabla ya watu hawajaweka makazi maeneo hayo lakini ilipaswa kutambua juu ya umuhimu wa afya na mazingira na sio kuwatupia lawama wananchi kwa kujenga makazi yao karibu na maji taka. Jukumu lao ni kuwasaidia wananchi na pengine kuihamasisha serikali ili wananchi hao waweze kuhama mahali hapo na kuwaelimisha wakazi hao.


Halmashauri husika za jijini zimezuia ubebaji hovyo wa taka ambapo baadhi ya watu hususan vijana hujiajiri kwa kupita majumbani mwa watu na kubeba taka na kisha huenda kuzitupa sehemu isiyo rasmi jambo ambalo ni kero kwa wengi kwani mara nyingi husubiri nyakati za usiku na kuzitupa taka hovyo katika misingi ya barabarani, nyumba za ibada na hata majumbani mwa watu. Utekelezaji wa jambo hili bado haujafanikiwa kwani serikali imekataza bila kuweka njia mbadala.

Licha ya kuwepo kwa magari maalum ya kubeba taka lakini kumekuwa na usumbufu mkubwa sana katika huduma hiyo. Kwanza magari ni machache na hayapiti pembe zote za jijini isitoshe hayana ratiba maalum, kwani unaweza kukaa miezi miwili bila kuliona gari hilo likipita kuchukua uchafu. Hii inapelekea ugumu kwa wakazi kuvumilia uchafu wenye harufu kali ndani ya mwezi mzima na ndio maana wengi hutumia njia zisizofaa ili kuweka nyumba zao katika hali ya usafi.

Hivi hizi ratiba hewa za haya magari huwa ni sehemu zote za jiji hata Masaki na Osterbay au ni kwetu tu mwananyamala kwa walalahoi? Ina maana hata viongozi nao hukaa na uchafu kwa muda usiojulikana? Kama mwendo ndio huo ni vema kwani naamini kuwa viongozi nao watakuwa wanatumia shortcut kutupa taka zao na wanajua fika kuwa hata iweje jiji haliwezi kuwa safi.

Kwa upande wa elimu inayotolewa kila mara na serikali na mashirika binafsi bado haijafaulu kwani elimu hii imekuwa ikitolewa bila kuangalia chanzo halisi cha uchafu wa jijini. Tatizo si msongamano wa watu pekee tatizo ni miundombinu mibovu, ufuatiliaji mbovu wa sera na umasikini, na umasikini ni sababu kuu mojawapo lawama zisitupwe tu kwa wananchi bila kuisahau serikali. Hata ukiwaambia watanzania waache kutupa taka hovyo je, serikali imewawezesha katika nyanja zote? Sio kuwaambia waache kutupa taka hovyo bila kuwawekea njia mbadala.

Hata hivyo elimu kwa wananchi pekee haitasaidia bali hata viongozi nao waelimishwe kwani tabia ya kutuletea magari yanayopita mara moja baada ya miezi tumeichoka na kama ratiba hizi ni kona zote za jiji hadi wanakoishi viongozi wetu ni wazi kuwa na viongozi wetu nao hawana elimu ya kutosha juu ya usafi. Inatakiwa sisi na viongozi tujifunze kuthamini chakula na yale yatokanayo na chakula ili kuimarisha usafi.

Kutokana na mfumo mpya wa serikali wa kuunda tume ili kuchunguza mambo mbalimbali naona sasa kuna umuhimu wa serikali yetu kuunda tume ili kuchunguza chanzo cha uchafu jijini labda hali ya usafi wa jiji hili unaweza kuimarika muda wote na sio kipindi cha akina Bush na wageni maarufu wanapotaka kuja nchini.

No comments: