Thursday, October 23, 2008

Nani anayestahili kuwa msanii na kuchambua kazi za wasanii?

Ingekuwa watanzania wengi wanaelewa maana ya sanaa ni wazi kuwa sanaa yetu ya Tanzania ingekuwa katika kiwango cha kimataifa. Ni dhahiri mtu atajiuliza kuwa, mbona filamu nyingi za kitanzania zinatungwa na idadi ya wasanii hususan wa muziki huongezeka kila uchao wa jua lakini eti mimi nasema watanzania wengi hawaelewi ni nini sanaa?.

Ni rahisi kuwasikia wasanii wenyewe wakijipongeza kutokana na kasi ya ukuaji wa sanaa huku na jamii nayo ikiwa na matumaini kuwa sasa Tanzania inaingia katika soko la kimataifa katika sanaa. Lakini husahau kuwa ongezeko la wasanii halimaanishi kuwa sanaa ya bongo inakua na badala yake wimbi kubwa la ongezeko la wasanii wetu linachangia kuporomoka kwa fani hii kitaalamu.

Wengi huiona sanaa kama ni kazi rahisi kuliko kazi zote ulimwenguni na mtu yoyote anaweza kuwa msanii au jaji wa kazi za sanaa. Kwa Tanzania mtu yeyote mwenye pesa anaweza kutengeneza kitu kinachoitwa filamu au kuwa producer kwa kuanzisha studio binafsi. Hili ni kosa kubwa ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya sanaa hapa nchini.

Tofauti na nchi zilizoendelea ambapo wao huiona sanaa kama ni taaluma na kumuona msanii kama ni mtu mwenye taaluma na kipaji Fulani, ndio maana wao Huiheshimu kazi hiyo, na huamini kuwa ili mtu aitwe msanii lazima awe na ujuzi alioupata kutokana na kile alichosomea mbali na kipaji. Hali hii hufanya kazi za wasanii wa nje kuonekana ni bora na kukaa kwenye chati muda mrefu kuliko kazi za wasanii wetu.

Kwanza kabisa wasanii wetu wengi hawana elimu juu ya kile wanachokizalisha. Waigizaji wengi wa Tanzania huokotwa, yaani mtu yeyote mwenye pesa anapotaka kutengeneza filamu hutafuta watu ambao yeye anaona kuwa wanaweza kuigiza na sio kuwa wana ujuzi au uzoefu wa kucheza filamu, na mtu huyo mwenye pesa yeye huwa kama director.

Kinachofanyika hapa ni uwezo wa kipesa ndio unaompa kiburi na sio utaalam. Sasa huyo director mwenyewe hana utaalam matokeo yake kinachoonekana kwenye filamu hiyo ni dhahiri kabisa kuwa utaona watu wakiigiza kwa vile wamekariri maneno na sio wameelewa wanaigiza kitu gani.mfano hebu angalia filamu hizi “usikose kwenye mazishi yangu na Laheri” waigizaji wake wote nawamekariri maneno hali inayomboa mtazamaji kwani haimpi msisimko mtazamaji wa filamu hizi, tofauti na unapongalia filamu za nje kama vile “remember your mother”, “Prison break” na nyinginezo nyingi.

Uhalisia wa maisha ya kitanzania hauonekani katika filamu nyingi za kibongo. Wengi wa wanaotengeneza filamu huiga uhalisia wa maisha ya ughaibini au ya kinigeria. Wengi huonesha maisha ambayo watanzania hawaishi.

Hata wasanii wetu wanapoamua kuigiza juu ya tamaduni za kitanzania basi mara nyingi sana hutumia tamaduni za kinigeria kuanzia mavazi hadi destuei ni za kinigeria. Mnigeria anapoangalia filamu hizi moja kwa moja atajua ni jamii yake ndiyo inayozungumziwa. Hivi ina maana watanzania hatuna utamaduni wa makabila yetu licha ya kuwepo makabila zaidi ya 100 hapa nchini?.

Hawa waigizaji kutuletea maisha ya kigeni kuanzia mavazi hadi utamaduni, kitu ambacho hukikuti katika jamii zetu ina maana wao hawajui hali halisi ya Tanzania, wanavyoishi watanzania, na changamotop zinazowakabili?.

Kipi ambacho katika filamu zetu za bongo mkulima anayetumia jembe la mkono, mpiga debe na mmachinga anaweza kunufaika nacho?. Filamu hizi zitaibua lini masikio ya mafisadi? Zitaibua lini jamii ambazo bado zina mila zisizofaa kama ukeketaji, Zitamuibua lini mlalahoi anayeishi chini ya dola moja kwa siku na kumsaidia?

Hatuoni wakiigiza jinsi wakulima wanavyopata tabu katika kilimo na hata katika uuzaji (soko), jinsi wamachinga wanavyopigwa kila siku na wanamigambo na jinsi ndugu zetu wakulima na wafugaji wanaopigana kila siku kwa sababu ya ardhi.

Ni mambo mengi ambayo yangewezwa kutengenezewa filamu Tanzania ili kuwaelimisha watanzania na kuwaburudisha kulingana na kuwa na uhalisia zaidi wa kitanzania na sio wa kigeni.

Soko huria nalo linaharibu fani hii kwani kuwepo na uhuru wa mtu yeyote kutengeneza filamu au kuwa producer, jaji na hata msanii bila kuangaliwa kama ana vigezo au la kumetuletea mambo yote haya ya kuvuruga sanaa. Kwani hakuna chombo chochote kinachohakiki kazi ya sanaa kabla ya kuingia sokoni.

Endapo kazi hizi zingekuwa zinafanyiwa utafiti na kusajiliwa na wataalam waliobobea katika fani hii tusingeona kazi zisizokuwa na mwelekeo na wasanii wangekuwa wachache na wanaheshimika. BASATA ina jukumu kubwa la kuifufua hadhi ya sanaa hapa nchini kwa kufuata mawazo haya.

Ningependa hadhi ya sanaa irudishwe nchini, tuna wasomi wengi chuo kikuu cha Dar es salaam katika idara ya sanaa na vyuo vingine vya sanaa hapa nchini, nadhani wanajukumu la kuikomboa sanaa ya Tanzania kama kweli wataweka nia ya dhati ya kuikomboa fani hii wanayoisomea kwa muda mrefu.

Huwa kila siku najiuliza mbona kila mwaka UDSM inatoa wataalamu wa sanaa lakini kinachofa nyika ni mauaji ya fanii hii na sio maendeleo? Wataalamu wetu wanaenda wapi au ndio wanakimbilia nje kwa ajili ya maslahi? Hapana wasifanye hivyo lazima waungane waketi na kisha watafakari wataiinua vipi sanaa ya Tanzania kwani kukimbia nchi sio suluhisho. Wote tukikimbia nani atabaki kuwa mtanzania mzalendo na kuikomboa sanaa hii?

Tukirudi katika muziki hususan Bongo Flava mambo ni yaleyale. Tatizo la elimu bado linajitokeza miongoni mwa wasanii wengi. Nikisema elimu simaanishi kuzungumza kiingereza, maana siku hizi wasanii wanaona ili kutoa kale kanakoitwa ujinga na kuonekana mjanja na msomi ni kujua kiingereza na sasa wasanii wengi wanazungumza lugha hii hata zaidi ya wasomi, tena sifa eti hata wanapohojiwa hujidai kuwa hawafahamu Kiswahili vizuri kwa kuchanganya na msamiati wa kiingereza.

La hasha! Mimi namaanisha elimu juu ya muziki. Ukiangalia kwa umakini na kwa undani zaidi wasanii wa bongo nao ni kama waigizaji wa filamu, wengi huimba muziki kwakuwa wana pesa au studio. Lakini vilevile wengi hujiunga na muziki baada ya kushindwa maisha. Yaani wengine hushindwa shule au kujikwamua kimaisha kutoka katika dimbwi la umasikini kwa kutumia njia nyingine na kuamua kuingia katika fani ya muziki.

Hapa wengi wao huuona muziki kama vile ni kitendo cha kuimba. Hawajui hata historia ya muziki mambo yaliyomo katika muziki na katika dunia ya leo ya utandawazi msanii anawezaje kukaa katika chati na kupata tuzo za kimataifa ndio maana nyimbo nyingi za bongo hupanda na kushuka chati haraka tofauti na miziki ya wenzetu.

Kwa haraka haraka kama ni mfuatiliaji mdogo wa muziki kama mimi, juzijuzi tu wimbo wa matonya uitwao “Anita” ulikuwa katika chati na ulikuwa unasikika karibu kila baada ya dakika 15 katika vituo mbalimbali vya radio na TV hapa nchini lakini leo hii hata siku tano zinapita bila kuusikia na ndio hata mwaka haujaisha na hata unapopigwa tena watu wanasikiliza lakini si kwa hamasa kama hapo awali.

Hata unapoangalia kumi bora katika za EATV kama kituo cha television kinachohusu burudani zaidi nyimbo nyingi zilizomo kwenye chati ni za ughaibuni. Hebu tutumie mfano huu pasi na kuangalia wanaopanga kumi bora hizo kama wana uelewa na fani ya muziki au la! Hata kama hawana uelewa kwanini nyimbo nyingi zinazoshika chati ziwe za ughaibuni na sio za bongo na kwanini nyimbo za bongo zishuke chati haraka tofauti na za huko magharibi? Tatizo ni nini na ile hali wote ni wasanii?

Hapa tatizo bado ni lilelile, watu hawaheshimu kazi za watu na ndio maana watu wengi wanaghushi kazi za wasanii na hupita barabarani bila wasi ni kwakuwa anayefenya kazi ya muziki anachotaka ni pesa ya kula mengine hajali, na akishanunua gari na kujenga kijumba kimoja anaona kashinda maisha na ni msanii bora kumbe anatakiwa aipandishe heshima kazi yake, kwake yeye akishapata ni sawa na waswahili wasemavyo “masikini akipata matako hulia mbwata”.

Sisemi hivi eti kwa kuwafagila wanaoghushi kazi za wasanii ila ni kwa kuwahurumia wasanii kwani huko tunakoeleka ni kugumu zaidi kama wasanii hawawatataka kujiona wasanii, kuthamini kazi zao na kuziwekea heshima basi jamii haitaziheshimu na badala yake kila siku wasanii wataishia kulia.

Sasa umefika wakati kwa Tanzania kuheshimu na kuthamini taaluma za watu si kila fani ionekane ni uzushi. Tunajua wazi kuwa japo sanaa inahitaji elimu lakini pia ni kipaji sasa sio wote tuna vipaji na hao wenye vipaji waviboreshe kwa elimu ili na sisi walau hata siku moja tuchukue tuzo ya muziki au filamu bora duniani.

Ili kuwasaidia wasanii hata waendeshaji wa vipindi vya muziki na sanaa kwa ujumla redioni na kwenye TV lazima wawe na ujuzi kwani na wao wanachangia sana kuporomoka kwa taaluma na fani hii nchini. Utakuta mtu eti kwakuwa ni mtangazaji basi hata ujaji wa sanaa anauweza. Tatizo si kujua kuongea na ujanja wa mjini matokeo yake utakuta msanii anasifiwa pasi na sifa.

Na pia waandaji wa tuzo za muziki au filamu nao wanatakiwa wawe ni wenye kuwa na ujuzi juu ya taaluma au fani hiii muhimu duniani.

Ni vema wasomi nao wakatia nguvu hili. Na endapo kutakuwa na bodi ya kuhakiki kazi za wasanii ni wazi kuwa hata hao wanaojiita maprodyuza ambao hawana ujuzi hawatakuwepo na watasoma na sasa sanaa yetu ya Tanzania itakuwa na sura mpya ulimwenguni.

No comments: